Alhamisi 26 Novemba 2026 - 10:30
Wanazuoni wa Kishia Katika Historia Yote Wamekuwa Kimbilio la Waliodhulumiwa na Vinara wa Mapambano Dhidi ya Dhuluma

Hawza/ Hujjatul-Islam wal-Muslimin Wa’izi amesema: Mkutano wa kuunga mkono wanazuoni wa Bahrain na Kuwait ni fursa ya kutangaza mshikamano na wanazuoni wa dini wanaopambana, pamoja na kulaani mashinikizo na hukumu za mahakama zilizotolewa dhidi yao.

Kwa mujibu wa mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Ahmad Wa’izi, Mkuu wa Ofisi ya Tabligh ya Hawza ya Kielimu ya Qom, jana Jumatano, katika Mkutano wa Kuunga Mkono Wanazuoni wa Bahrain na Kuwait, akizungumzia malengo ya kufanyika mkutano huo, amesema: “Falsafa ya mkutano huu ni kuonesha huruma, mshikamano na kutangaza heshima ya Hawza ya Kielimu ya Qom kwa wanazuoni wa dini wanaopambana, ambao kwa sasa wako katika mstari wa mbele wa mapambano dhidi ya ufisadi, dhuluma na uharibifu, pamoja na kukabiliana na mkondo wa ubeberu, huku wakiwa katika magereza ya Bahrain na Kuwait.”

Mjumbe wa Baraza Kuu la Mapinduzi ya Utamaduni, akieleza kwamba; wanazuoni wa Kishia katika historia yote wamekuwa daima kimbilio la wanyonge na waliodhulumiwa, ameongeza: “Mbali na majukumu yao ya kielimu, kimaadili, kimaarifa na ya uongozi, wanazuoni wa dini daima wamekuwa wakitekeleza pia jukumu lao la kijamii kwa kuwaunga mkono watu waliodhulumiwa na kutetea haki zao. Nafasi hii ni miongoni mwa fahari kubwa za wanazuoni wa Kishia katika historia yote.”

Hujjatul-Islam wal-Muslimin Wa’izi, akirejelea wosia wa Amirul-Muuminina Ali (a.s.) kwa wanawe, ambao alisema:

«کونا لِلظّالِمِ خَصماً وَلِلْمَظْلُومِ عَوْناً»

“Kuweni maadui wa madhalimu na wasaidizi wa waliodhulumiwa.”

Alikumbusha wasia huo na kusisitiza: “Kusimama pamoja na waliodhulumiwa na kukabiliana na madhalimu, kwa hakika ni kuitikia wito wa wosia wa kiongozi wa wachamungu. Leo hii, wanaokabiliana na wanazuoni wa dini wa kweli nchini Bahrain na Kuwait ni serikali tegemezi na za mrengo wa nyuma, pamoja na mkondo wa ubeberu wa kimataifa. Jambo hili lenyewe linaonesha ukweli na usahihi wa njia na shughuli za wanazuoni wanaopambana katika nchi hizi mbili.”

Mkuu wa Ofisi ya Tabligh ya Hawza ya Kielimu ya Qom, akisisitiza kwamba wanazuoni wa dini bado wako katika mstari wa mbele wa kuongoza, kupambana na kufanya Muqawama dhidi ya ukafiri na Taghuti, amebainisha: “Nafasi hii inaonesha kwamba wanazuoni wa dini wa kweli, hata katika mazingira magumu, hawajaacha jukumu lao la kihistoria la kutetea haki na kuwaunga mkono waliodhulumiwa.”

Aidha, akizungumzia ahadi ya Mwenyezi Mungu ya kuwasaidia Waumini, amesema: “Imani na yakini katika ahadi ya haki ya Mwenyezi Mungu, yaani aya tukufu isemayo:

«إِن تَنصُرُوا اللَّهَ یَنصُرْکُمْ وَیُثَبِّتْ أَقْدَامَکُمْ»

‘Mkimnusuru Mwenyezi Mungu, naye atakunusuruni na kuithibitisha miguu yenu.’

Inapaswa kuwa daima taa inayowaongoza wanamapambano na wapigania haki. Hii ni kwa sababu Mwenyezi Mungu ameahidi kuwasaidia wale wanaopiga hatua katika njia ya kuinusuru dini na haki, na kuifanya miguu yao kuwa imara.”

Hujjatul-Islam wal-Muslimin Wa’izi, ili kufafanua ukweli huu, alirejelea baadhi ya matukio katika maisha ya Imam Shahidi na kusema: “Je, wakati alipokuwa katika magereza na uhamisho mbalimbali, huku akiwa amejitayarisha kuvumilia matatizo na hata kufikia shahada, alikuwa anadhani kwamba siku moja angefikia nafasi ambayo kupitia juhudi na msimamo wake thabiti mbele ya madola makubwa ya kijeshi duniani, angekuwa fahari kwa Mashia na historia ya Uislamu?”

Akaendelea kusema: “Mwenyezi Mungu alimpa daraja na heshima kubwa mwanamapambano aliyesimama kwa ajili ya kutafuta radhi Zake, ambaye hata kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu alikuwa tayari kujitoa mhanga. Alimpa hadhi kiasi kwamba kwa kipindi cha miaka 37 aliweza kuwa na mchango katika kuimarisha zaidi mfumo wa Kiislamu, na kuipa Iran na watu wake, Ushia na ulimwengu wa Kiislamu utukufu na adhama. Mfano huu unaonesha kwamba mwisho wa mapambano katika njia ya Mwenyezi Mungu huwa zaidi ya hesabu za kawaida za kibinadamu na za kidunia.

Mkuu wa Ofisi ya Tabligh ya Qom, pia akizungumzia kipindi cha upweke na uhamisho wa Imam Khomeini (r.a.), pamoja na tukio la Kuwait kumzuia kuingia nchini humo, amesema: “Picha iliyopigwa ya Imam Khomeini (r.a.) akiwa anatawadha katika mpaka wa Kuwait inadhihirisha upweke na matatizo aliyovumilia katika njia ya mapambano. Lakini ni nani aliyewahi kufikiria kwamba Mwenyezi Mungu angemfikisha mtu huyo aliyekuwa mpweke katika nafasi ambayo Marji’ wa Taqlidi na mwanazuoni wa dini angeweza, kwa mara ya kwanza katika historia ya Ushia, kuanzisha mfumo ambao ungesimama dhidi ya ukafiri na ubeberu wa kimataifa, na kuurudishia Uislamu na Waislamu heshima na adhama?”

Hujjatul-Islam wal-Muslimin Wa’izi, akisisitiza kwamba mabadiliko na hatima ya mapambano havipaswi kupimwa kwa kutumia hesabu za kimada pekee, amebainisha: “Ingawa katika hesabu za kidunia inaweza kuonekana kwamba mazingira yote yanaunga mkono upande wa ubeberu, lakini Mwenyezi Mungu amezunguka kila jambo kwa ujuzi Wake, na mipango pamoja na makadirio ya ulimwengu yako mikononi Mwake. Jambo muhimu ni kuwa na imani ya kweli katika ahadi ya Mwenyezi Mungu na kusimama imara katika njia ya haki.”

Mwisho, akionesha matumaini yake kuhusu ushindi wa upande wa haki na kuachiliwa huru wanazuoni waliofungwa nchini Bahrain na Kuwait, amesema: “Tunatumaini kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu ataujalia hivi karibuni upande wa haki ushindi na msaada Wake. Na kwa baraka za Mtukufu Muhammad (s.a.w.w.), familia Yyake tukufu na Bibi Swiddiqah Tahirah (s.a.), atafanikisha kuachiliwa huru wapendwa hawa, na kushindwa ukafiri wa kimataifa pamoja na ushindi wa Umma wa Kiislamu, atazifanya nyoyo za Waislamu zifurahi.”

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha